Wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiadhimisha mwaka mmoja sasa tangu kutiwa mikononi ndege ya kisasa ya kijasusi ya Marekani aina ya RQ-170 huko mashariki mwa Iran, hii leo tarehe 4 Disemba kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limetangaza kuwa limefanikiwa kunasa ndege nyingine ya kijasusi ya Marekani aina ya ScanEagle katika maji ya Ghuba ya Uajemi.
Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran Admeri Ali Fadavi amesema kuwa wataalamu wa jeshi hilo wamefanikiwa kushusha chini na kuinasa ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani ambayo imeingia katika anga ya Iran ikiongozwa kutoka mbali. Ripoti zinasema kuwa, ndege hiyo ya Marekani siku kadhaa zilizopita ilinaswa na wanamaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada tu ya kuingia katika anga ya Iran ikiwa katika operesheni ya kijasusi ya kukusanya ripoti na habari katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Admeri Fadavi anasema ndege hiyo isiyo na rubani ni aina ya ScanEagle ambayo kwa kawaida hurushwa kutoka kwenye manoari kubwa za kivita. Ndege hiyo ina umbo dogo na haibebi silaha na hutumiwa na kikosi cha operesheni maalumu za kijeshi.
Ndege zisizokuwa na rubani za Marekani zimekuwa zikikaribia mipaka ya angani ya Iran na kujaribu kukusanya habari na ripoti za kijasusi lakini mara zote zinakabiliwa na jeshi la Iran. Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran Admeri Ali Fadavi anasema kuhusu utayarifu wa jeshi la mawanamaji wa Iran kuwa, jeshi hilo liko katika hali nzuri kabisa ya kukabiliana na hujuma za adui.
Ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya ScanEagle ni ndege ndogo iliyotengenezwa na kampuni ya Insitu ambayo ni miongoni mwa mashirika tanzu ya Boeing. Drone hiyo ina darubini ya electro-optical na infrared na ina uwezo wa kufikisha mawasiliano umbali wa zaidi ya kilomita mia moja. Inaweza kupaa angani kwa zaidi ya masaa 20 na kwenda mwendo wa kasi ya kilomita 120 kwa saa.
Mwezi uliopita ndege nyingine isiyo na rubani ya Marekani aina ya Predator ililazimika kukimbia haraka na kuondoka katika anga ya Iran kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi baada ya kuandamwa na ndege za kivita za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Wiki kadhaa zilizopita pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilisha barua rasmi katika Umoja wa Mataifa ambayo mbali la kulaani uchokozi huo wa Marekani, imeutaka umoja huo kuzuia chokochoko hizo za Washington.
Habari hiyo ya kunaswa ScanEagle ilitangazwa na vyombo vyote muhimu vya habari duniani muda mfupi tu baada ya Iran kutangaza kwamba jeshi lake limeinasa katika anga yake kwenye Ghuba ya Uajemi
ConversionConversion EmoticonEmoticon