Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu
wa Jimbo la Urambo Tabora Samwel Sitta.
Mzee Samwel Sitta
amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical
University of Munich Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi
uliopita.
Katika
salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko
makubwa taarifa za kifo cha Samwel Sitta na Taifa limempoteza mtu muhimu
aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Nitamkumbuka
Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya
kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi
mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia
kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe.
Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya
marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi
wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli
amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha
maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Taarifa imetolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU. Dar es Salaam
07 Novemba, 2016
INTERVIEW: Haya hapa chini ni mahojiano ya mwisho ya Mzee Samwel Sitta na millardayo.com na AyoTV na alikua akikanusha taarifa zilizoandikwa gazetini kwamba amehamishwa kwenye nyumba ya serikali aliyokua akiishi.
ConversionConversion EmoticonEmoticon