Serikali iainishe viwanda vinavyohitajika’


SERIKALI imeshauriwa kuainisha aina ya viwanda vinavyotakiwa nchini, kupunguza bei ya umeme, kuondoa urasimu na baadhi ya kodi, vinginevyo kuna viwanda vitaanzishwa na kufungwa baada ya muda mfupi.
Ushauri huo ulitolewa bungeni hapa na Mbunge wa Meatu, Salum Hamisi Salum (CCM) wakati akichangia Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/17.
“Ni lazima tuainishe tunataka kuanzisha kiwanda gani, mahala gani na kwa ajili ya soko lipi, kwani kuna viwanda haviwezekani kuanzishwa hapa nchini,” alisema Salum maarufu kama Mbuzi.
Mbunge huyo ambaye pia ni mmiliki wa viwanda, alisema amelazimika kufunga viwanda vyake saba alivyovianzisha kwa gharama kubwa kutokana na mazingira mbalimbali.
Alitoa mfano wa kiwanda cha nyuzi cha kisasa alichoanzisha kwa mitambo kutoka Ujerumani ambacho amelazimika kukifunga kwa sababu kimekuwa kikimuingizia hasara kwa kushindwa kushindana kwenye soko.
“Tatizo la kwanza ni umeme. Umeme wetu bado ni ghali kulinganisha na kwingineko; kuna kodi, gharama za nguvu kazi na urasimu mwingi kwa kuwa hapa Tanzania kila mtu ana maamuzi. Sasa unazalisha nyuzi kwa gharama kubwa, lakini unakuta sokoni na wenzako wana bidhaa hiyo hiyo lakini wamezalisha kwa gharama za chini. Hapo lazima utafunga kiwanda,” alisema.
Wakati huo huo, Mbunge wa Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa (CCM), ameitaka serikali kuharakisha ujenzi wa Bandari ya Bagomoyo akisema ni vyema ujenzi huo uende sambamba na ule wa reli ya kisasa, kwani ni vitu vinavyoshabihiana.
Alisema anachojua yeye, wabia katika ujenzi huo kwa maana ya nchi za China na Oman wako tayari, lakini ni sisi Tanzania ndio tunaosuasua. Alitaka pia serikali iharakishe kuwalipa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo ambayo alidai ikikamilika kama ilivyopangwa itaifanya Tanzania kuwa Singapore ya Afrika.
Previous
Next Post »