Melania Trump ashtaki gazeti kuhusu tuhuma za ukahaba

Melania Trump

Melania Trump amelishtaki gazeti la Daily Mail la Uingereza pamoja na mwanablogu wa Marekani akitaka alipwe $150m (£114m) kuhusiana na tuhuma kwamba alikuwa kahaba miaka ya 1990, wakili wake amesema.
Gazeti la Daily Mail lilidokeza kwamba huenda Trump alifanya kazi ya muda kama kahaba New York, na kwamba alikutana na mumewe Donald Trump, ambaye kwa sasa anawania urais, mapema kuliko inavyodaiwa.
Mwanablogu Webster Tarpley aliandika kwamba Bi Trumpa anahofia sana maisha yake ya awali yasifichuliwe kwa umma.
Madai hayo ni "uongo mtupu, wakili wake Charles Harder amesema.
"Washtakiwa walitoa tuhuma kadha kuhusu Bi Trump ambazo ni za uongo 100% na kumharibia sana sifa," Bw Harder alisema kupitia taarifa.
Bi Trump, 46, alizaliwa Slovenia na akahamia Marekani kufanya kazi kama mwanamitindo miaka ya 1990.
Aliolewa na Bw Trump mwaka 2005.
Gazeti la Daily Mail lilinukuu madai yaliyokuwa yamechapishwa na jarida moja la Slovenia kwa jina Suzy kwamba wakala wa uanamitindo ambaye Bi Trump alikuwa akifanyia kazi wakati huo pia alihudumu kama wakala wa kutafutia kazi makahaba, nyaraka za mahakama zinaonesha.
Gazeti hilo pia lilimnukuu mwanahabari wa Slovenia Bojan Pozar, ambaye aliandika kitabu kuhusu maisha ya Bi Trump ambacho hakijaidhinishwa, ambaye alidai kwamba Bi Trump alipigwa picha za utupu New York mwaka 1995 na akadai kwamba mwanamke huyo alikutana na Bw Trump miaka mitatu kabla ya wakati ambao inadaiwa walikutana, ambayo ni mwaka 1998.
Wakili wake anasema alihamia Marekani mwaka 1996.
Bw Tarpley pia alidai kwamba Bi Trump ana wasiwasi sana kwamba huenda 'wateja wake matajiri' wa wakati huo wakafichua siri yake na kwamba alikuwa na mfadhaiko.
Bw Tarpley na Daily Mail wote walibadilisha taarifa zao baadaye.
Previous
Next Post »