UN yahimiza kuwepo utulivu Gabon

Gabon


Umoja wa Mataifa umezihimiza kuwepo kwa utulivu nchini Gabon baada ya fujo kuzuka kuhusiana na utata kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.
Baraza la Usalama la umoja huo limetoa wito kwa wagombea wakuu na wafuasi wake kujizuia kufanya uchokozi na kutatua mzozo wa sasa kupitia njia za kisheria.
Maafisa wa usalama kufikia sasa wamewakamata watu zaidi ya elfu moja baada ya siku ya pili ya maandamano ya wafuasi wa upinzani.
Upinzani unadai Rais Ali Bongo aliiba kura wakati wa uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi.



Bongo na Ping
Rais Bongo amesisitiza kwamba alishinda kwa njia halali na kuutaja ushindi wake kuwa ushindi wa watu wa Gabon.
Amesema kuna kundi ndogo la watu wachache waliotaka kutwaa madaraka na ambao wameshindwa.
Matokeo ya uchaguzi yalitangazwa Jumatano alasiri na kumpatia Bw Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura, akifuatwa na Bw Ping aliyepata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.
Bw Ping alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na "hakuna ajuaye" hasa nani alishinda.

Fujo Gabon
Upande wa Bw Ping unasema takwimu kutoka ngome za rais huyo zinaonyesha asilimia 99 ya wapiga kura walijitokeza. Ameomba takwimu za wapiga kura kutoka kila kituo zitolewe wazi.
Bw Bongo aliingia madarakani mwaka wa 2009, baada ya kifo cha babake aliyekuwa ameongoza taifa hilo tangu 1967.
Kabla ya kuingia katika siasa, Ping aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
Previous
Next Post »