Nafasi iliyopata Tanzania kwenye Jumuiya ya SADC

Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali umemalizika katika mjini Mbabane Swaziland ambapo Tanzania imeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi muhimu na nyeti ya Siasa, Ulinzi na USalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika- ‘SADC’ ambapo nchi ya Angola imeteuliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa asasi hiyo.
Akizungumzia mjini Mbabane – Swaziland, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye alimwakilisha Rais Magufuli amesema kuwa nchi wanachama wa SADC kwa sasa zinatakiwa kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi haraka kama hatua ya kujenga ustawi bora wa wananchi wa kanda hiyo.
Kuhusu Tanzania kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa nchi za SADC, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt Augustine Mahiga amesema Tanzania itahudumu katika asasi hiyo kwa mwaka mmoja na ana imani kuwa changamoto za kisiasa zilizopo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Lesotho zipatiwa ufumbuzi.
Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC pia umeiteua nchi ya Swaziland kuwa mwenyekiti wa SADC na Jamhuri ya Afrika Kusini imeteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC.
Katika mkutano huo wakuu wa nchi na serikali wametia saini rasimu za maboresho ya mikataba mbalimbali ya jumuiya hiyo ikiwemo mkataba wa kuboresha itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya itifaki ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama ya SADC na maboresho ya itifaki ya biashara.
Previous
Next Post »