Juzi Yanga iliifunga Stand United mabao 3-1 katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, matokeo ambayo yaliiweka Yanga jirani kabisa na ubingwa baada ya kufikisha pointi 68. Kwa matokeo ya juzi, Yanga ilikuwa ikihitaji pointi nne tu ili iwe bingwa kwani ingefikisha pointi 72 ambazo hakuna timu ambayo ingeweza kuzifikia.
Lakini kutokana na matokeo ya jana, Yanga sasa inahitaji pointi tatu tu kuibuka bingwa, kwani itafikisha pointi 71 ambazo hakuna timu itakayozifikia. Azam inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 60, kama itashinda michezo yake iliyosalia itafikisha pointi 69, wakati Simba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 58 ikishinda michezo yake minne iliyosalia itafikisha pointi 70.
Yanga imebakisha mechi zote ugenini dhidi ya Mbeya City ya Mbeya, Ndanda FC ya Mtwara na Majimaji ya Songea. Pia matokeo ya jana, yameisaidia JKT Ruvu ambayo imefikisha pointi 26 na kupanda nafasi moja ikitoka ya 14 hadi ya 13 katika timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.
JKT Ruvu imebakisha michezo mitatu. Katika mchezo wa jana, Azam ilipata bao la kwanza dakika ya 31 mfungaji akiwa Michael Balou baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa wapinzani wao.
Dakika saba baadaye Kipre Tchetche aliifungia Azam bao la pili akimalizia kazi nzuri ya Mudhathir Yahya. JKT Ruvu ilipata bao la kwanza dakika ya 57 mfungaji akiwa Saad Kipanga kwa penalti baada ya beki Gadiel Michael kuushika mpira katika eneo la hatari. JKT Ruvu ilisawazisha bao dakika ya 71 mfungaji akiwa Mussa Juma kwa shuti baada ya kipa Aishi Manula kuutema mpira.
ConversionConversion EmoticonEmoticon