Yanga wamkuna Pluijm


KOCHA wa mabingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Hans van der Pluijm amewamwagia sifa wachezaji wake, akisema wamepigana kiume kutwaa ubingwa, akisisitiza haikuwa kazi nyepesi katika harakati za kutetea taji hilo.
Yanga imefanikiwa kutetea taji hilo baada ya kufikisha pointi 71, ambazo haziwezi kufikiwa na timu mbili zinazoifuatia, Azam na Simba, ambazo awali zilikuwa zikiipa presha kutokana na kutofautiana kwa idadi ndogo ya pointi.
Hii ni mara ya 26 kwa Yanga kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara tangu kuanzishwa kwa michuano ya ubingwa wa soka nchini mwaka 1965 na ndio mabingwa wa kihistoria wa ubingwa nchini, ikifuatiwa na Simba iliyotwaa mara 18.
Akizungumza na gazeti hili, kocha huyo raia wa Uholanzi, lakini aliyebobea katika soka ya Afrika, alisema walikuwa na vita kuu tatu hadi kufanikiwa kutetea ubingwa huo, lakini ameshinda kutokana na uimara wa kikosi chake alichokitengeneza kwa miaka miwili, lakini pia ushirikiano wa benchi la ufundi, uongozi na mashabiki.
Amezitaja vita hizo kuwa, moja ni ugumu wa ligi kutoka kwa timu shiriki, pili ni kupata majeruhi ya wachezaji muhimu katikati ya msimu na ya mwisho ilikuwa ni ugumu wa ratiba iliyotokana na ushiriki wao wa michuano ya kimataifa.
Mbali ya Ligi Kuu na Kombe la FA, Yanga inaiwakilisha pia nchi katika michuano ya kimataifa, awali ikianzia katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika raundi ya tatu, imeangukia katika Kombe la Shirikisho Afrika inakoelekea kufuzu kwa hatua ya makundi.
“Pamoja na upana wa kikosi chetu, kuna wakati tulilazimika kuwatumia wachezaji wagonjwa kwa kuwachoma sindano za ganzi, lakini pia ratiba ilikuwa ngumu na kikwazo ambacho tulidhani kingetuharibia malengo yetu, kwani kuna wakati tulicheza mechi tano kwa siku 10 tena tunasafiri umbali mrefu,” alisema Pluijm.
Pamoja na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, amewataka wachezaji wasibweteke kwani bado wanakazi kubwa ya kuhakikisha wanashinda taji la Kombe la FA na kufanya vizuri kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola.
Yanga, baada ya kuipiga Esperanca 2-0 mwishoni mwa wiki iliyopita, itarudiana nayo katikati ya wiki ijayo huko Angola, na endapo itashinda, itaingia katika hatua ya makundi ambayo itakuwa ya neema kwa timu shiriki kutokana na utajiri wa fedha unaomwaga kuanzia hatua hiyo.
Yanga kesho inatarajiwa kukabidhiwa Kombe lake la ubingwa wa Tanzania Bara Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, na kocha huyo alisema mafanikio yao ya msimu huu yametokana na kikosi bora walichokitengeneza kwa misimu miwili na hiyo ndiyo tofauti yao na timu 15 walizokuwa wakishindana nazo kuwania ubingwa huo
Previous
Next Post »