WIZARA ya Maliasili na Utalii imeridhia maombi ya Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa jeshi usu (Paramilitary) ili kukabiliana na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori, misitu, na rasilimali nyingine za nchi.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya askari na wahifadhi wa shirika hilo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maombi ya shirika hilo kutaka kubadilishwa na kuendeshwa kwa sheria za kijeshi ni ya msingi katika kipindi hiki ambacho Tanzania inakabiliwa na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori.
Ufungaji wa mafunzo hayo ulifanyika juzi katika kambi ya Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi mkoani Katavi ambako askari 101 na wahifadhi 26 walihitimu mafunzo ya kijeshi ya miezi mitatyu hadi sita “Kwa sasa uhifadhi unakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili,hususan tembo na faru kuporomoka kwa maadili ya askari na uingizaji wa mifugo hifadhini,” alisema Meja Jenerali Milanzi.
Aliongeza: “Maombi yenu yamekuja kwa wakati muafaka hivyo tutawasilisha katika mamlaka nyingine za juu za kiserikali, ili yatungiwe sheria na hatimaye kuwasilishwa bungeni ili yajadiliwe na kupitishwa kuwa sheria.”
Hata hivyo, aliwataka askari hao pamoja na Menejimenti ya Tanapa kufanya maandalizi ya kutosha kwa msingi kuwa sheria itakapopitishwa baadhi ya mambo yatabadilika na kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kijeshi kwa ilivyo kwa majeshi mengine nchini.
Awali akiwasilisha maombi hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alisema shirika hilo baada ya kutafakari kwa kina wakitumia wataalamu wa ndani ya shirika walibaini umuhimu wa askari wao kutumia sheria za kijeshi kutokana na changamoto ya sasa ya katika masuala ya uhifadhi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga alielezea umuhimu wa kutunza maeneo yaliyohifadhiwa huku akionya kuwa makundi ya wafugaji yanayovamia maeneo hayo lazima yaondolewe haraka
Previous
Next Post »