Chereko za ubingwa Yanga kufuru Taifa


YANGA imepanga kufanya sherehe kubwa za ubingwa kesho baada ya mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku ikisema italipitisha Kombe Mtaa wa Msimbazi kwa lengo la `kuwazindua’ watani wao wa jadi Simba waweze kuzinduka na kurejesha ushindani katika soka.
Yanga ilitwaa ubingwa tangu Jumatatu baada ya kuifunga Mbeya City kwa 2-0 mjini Mbeya.
Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema jana kuwa mechi hiyo wataitumia kama maandalizi kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperanca ya Angola katikati ya wiki ijayo.
Katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, Yanga ilishinda 2-0 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.
“Tumeshachukua ubingwa, bado kukabidhiwa kombe tu, shamrashamra ndio tunazianza, tumeomba ulinzi wa Polisi bado hawajatupangia barabara tutakayopita lakini mwisho wa siku lazima tupite Msimbazi kwa mahasimu wetu. “Lengo la kupita ni kuwahamasisha na wao msimu ujao wafanye usajili wa uhakika, ili tuwe wapinzani wa kweli, maana sasa hivi tumejikuta wapinzani na Azam sisi wapinzani wetu ni Simba, Yanga inachukua ubingwa, lakini haina furaha kuona mtani wake mambo si mazuri,” alisema Muro
Previous
Next Post »