Katika ripoti hiyo iliyofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kutolewa mapema wiki hii mjini Dodoma, inaonesha kuwa idadi ya walimu hao imeongezeka kutoka walimu 963 mwaka 2014 hadi kufika waalimu 2,108 mwaka jana. Ilieleza kuwa sababu kubwa ya kuwa na walimu wasio na sifa zaidi ya moja imetokana na Ofisi ya Waziri Mkuu (wakati huo), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kushindwa kuwa na mpango wa kuwaendeleza walimu waliowaajiri.
Ripoti maalumu hiyo ya ubora wa elimu nchini imebaini kuwa matarajio ya wengi ilikuwa ni kuona idadi ya walimu wasio na sifa ikipungua kutokana na wengi wao kustaafu na wengine wapya kuajiriwa ambao wana sifa, lakini cha ajabu idadi hiyo imeongezeka.
“Tulitegemea walimu wasio na sifa ambao ni waajiriwa wa muda mrefu muda wa kustaafu umefika na wengine walishastaafu, sasa tulitegemea hao wapya walioajiriwa wawe na sifa, lakini cha ajabu ndio wameongezeka wasio na sifa za kufundisha sekondari,” alisema CAG, Profesa Mussa Asaad.
Kwa mujibu wa vigezo vya walimu wenye sifa za kufundisha elimu ya sekondari nchini, mwalimu anatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha chini ambacho ni Stashahada ya Elimu kwa walimu wanaofundisha kidato cha kwanza hadi cha nne.
Kwa wale wanaofundisha kidato cha tano na sita, wanatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha Shahada ya Elimu iliyotolewa kwenye chuo kinachotambuliwa. Tofauti na masharti hayo, kwa mwaka jana ukaguzi maalumu kuhusu elimu ulibaini kuwa serikali kwa nyakati tofauti kutokana na uhaba wa walimu, iliamua kuajiri walimu wasio na sifa wakiwemo wale waliomaliza kidato cha sita na kuwapa kibali cha kufundisha kwa lengo la kuwaendeleza miaka ya baadaye.
Hata hivyo, ukaguzi huo ulibaini kwamba pamoja na walimu hao kupewa mikataba yenye kuonesha muda wa kufundisha wakiwa na elimu hiyo na kutakiwa kujiendeleza masomo ya ualimu kwa muda uliowekwa, wengi wao hawakufanya hivyo. Lakini pia ukaguzi huo ulibaini kuwa makosa yako pia Tamisemi ambao ndio walishindwa kuwa na mpango wa mafunzo kwa walimu kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 na hivyo walimu hao kuendelea kufundisha licha ya kutokuwa na sifa stahiki.
Pia imebainika kuwa wapo walimu wasio na sifa waliojiendeleza masomo ya elimu ya juu, lakini wakasoma fani tofauti na elimu, jambo ambalo ni kinyume cha matakwa ya vigezo vya sifa za ualimu na bado wameruhusiwa kuendelea kufundisha.
Katika mahojiano kati ya CAG na Tamisemi kuhusu uwepo wa walimu wasio na sifa, ripoti ilisema hatua zilishaanza kuchukuliwa kwa kutoa mwongozo kwa waajiri wote wa shule za msingi na sekondari nchini, kuajiri walimu wenye sifa na kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza walimu wasio na sifa.
Licha ya ukweli kwamba bado kuna uhaba wa walimu wenye sifa hususan kwenye masomo ya sayansi, CAG alisema takwimu zinaonesha kuwa mahitaji wa walimu wa sayansi ni asilimia 61 na waliopo sasa ni asilimia 39 tu.
Ripoti hiyo imebaini jambo jingine kuwa mgawanyo wa walimu kwenye mikoa mbalimbali kulingana na mahitaji haufanywi kwa kuangalia uwiano jambo lililosababisha kwa mwaka 2014, kuwepo na ziada ya walimu 2,960 wa masomo ya sanaa kwenye shule mbalimbali za sekondari nchini.
“Ukosefu wa takwimu ndio tatizo kubwa kwenye sekta ya elimu, mfano tu kwa mwaka 2014, walimu zaidi ya 2,960 wanaofundisha masomo ya sanaa walipelekwa kwenye shule zisizo na mahitaji ya walimu hao, huko maeneo yenye uhitaji yakiwa hayana walimu,” alisema CAG.
Hata hivyo, ripoti hiyo imebaini kuwa kwa miaka 10 iliyopita wapo walimu waliopaswa kujiendeleza ili kuwa wakufunzi ila hawajafanya hivyo huku wengine zaidi ya 405 waliopaswa kujiendeleza kwa masomo ya ualimu nao wakishindwa.
Pia wapo walimu 88 waliopewa kibali cha kufundisha na kutakiwa kujiendeleza kwa mafunzo ya ualimu, ila wamejiendeleza kwenye fani nyingine nje ya ualimu na wengine 317, taarifa zao za kujiendeleza hazijapatikana.
Aidha, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebainisha upungufu kadhaa katika manunuzi ndani ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART), jipu lingine limeibuliwa ndani ya mradi huo.
Jipu jipya ndani ya mradi huo ni lile la ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhia Mabasi ya Mradi huo katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam. Kujengwa kwa kituo hicho kumekuwa kukilalamikiwa na wananchi na hasa wakazi wa Dar es Salaam wakieleza kushangazwa na hatua hiyo hasa kutokana na serikali kuwahamisha wakazi wa eneo hilo la Jangwani kutokana na kudaiwa kujenga nyumba zinazochangia kutokea kwa mafuriko.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad amebainisha hayo alipozungumzia mchakato wa tathmini ya athari za mazingira katika miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa CAG, anayepaswa kubebeshwa mzigo huo wa kutozingatia athari za kimazingira katika ujenzi wa kituo hicho ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambalo alisema haieleweki ni kwa sababu ipi liliruhusu kujengwa kwa kituo hicho.
Katika ripoti yake, CAG alisema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira imeainisha aina ya miradi ya maendeleo inayotakiwa kufanyiwa tathmini ikiwa utekelezaji wake utaathiri mazingira. Alisema usimamizi wa tathmini ya athari zinazoweza kutokea katika mazingira ni muhimu katika kulinda mazingira na maslahi ya umma kwa ujumla.
Alisema lengo la ukaguzi wa CAG katika eneo hilo, ulilenga katika kutathmini iwapo Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira walisimamia kikamilifu mchakato wa tathmini ya athari za mazingira kabla ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Profesa Assad alisema katika ukaguzi huo walibaini NEMC haikuweza kutambua miradi yote iliyotakiwa kusajiliwa ili ifanyiwe tathmini na kwamba vibali mbalimbali vya uendelezaji wa miradi vilitolewa pasipo kuonesha uthibitisho kuwa Baraza limeridhia.
Alisema ukaguzi ulibaini pia, kulikuwa na kutohusishwa kwa wadau muhimu wakati wa kupitia nyaraka za awali zinazoelekeza miradi ilivyo hasa serikali za mitaa ambako miradi husika inatekelezwa.
“Tathimini za kimazingira hazikuweza kubaini masuala yenye athari kubwa kwa mazingira kama vile ujenzi wa kituo cha kuhifadhia mabasi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, katika eneo la Jangwani Dar es Salaam,” alisema Profesa Assad.
Akitoa maoni ili kuzuia kutokea kwa kasoro kama hizo mbeleni, alisema NEMC na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira wanatakiwa kusimamia ipasavyo mchakato wa tathmini ya athari ya mazingira au ukaguzi wa mazingira katika miradi ya maendeleo
ConversionConversion EmoticonEmoticon