Simba walia usaliti kuvurunda Ligi

UONGOZI wa Klabu ya Simba umetaja sababu mbalimbali zilizofanya wavurunde msimu huu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, huku sababu kubwa ikiwa ni usaliti wa baadhi ya wachezaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa Simba Evans Aveva, alisema kikosi chao kilikuwa na wachezaji wasaliti na ndio waliofanya klabu hiyo ishindwe kufurukuta na kutwaa ubingwa.
“Ni wanajeshi ambao hawakuwa tayari kutumikia jeshi letu, kuna mchezaji kwa makusudi au kimchezo alifungiwa kutokana na utovu wa nidhamu, tukaongeza adhabu ili kukomesha vitendo hivyo, lakini kabla ya msimu haujaisha ameshaondoka na kwenda kusajili timu nyingine. “Mwingine amefanya rafu, akapewa kadi nyekundu na usiku akatuma meseji anaondoka alfajiri alipokwenda mpaka sasa hatujui, lakini naweza kusema hawa ndiyo wachezaji waliotufikisha hapa.
“Wakati bado tunatafakari wakaibuka wengine kushawishi wachezaji wengine wasiende Songea, sababu mshahara haujalipwa, ni kitu cha kawaida kwa Simba na Yanga kupata mishahara tarehe 6 mpaka 10 na tulishawaeleza wachezaji na si mara ya kwanza mishahara kuchelewa…” alisema Aveva na kuongeza; “ Lakini kutokana na sababu ambazo wanazijua wao, sisi tumeona ni hujuma wameshawishi wachezaji wengine wasiende, nashukuru Mungu wengine walielewa na wakaenda safari.”
Hata hivyo, katika mazungumzo hayo hakutaja jina la wachezaji wasaliti zaidi ya kuonekana kuzungumza kwa mifano tu na kusisitiza kuwa Simba haiwezi kuvumilia kukaa nao. Pia alisema kuna tatizo kwa wachezaji wa kigeni na kusisitiza kuwa msimu ujao watahakikisha wanakuwa makini katika kusajili wachezaji wa nje.
Pia alisema mwaka huu walijitahidi kuboresha maslahi ya wachezaji kwa kuwapa fedha za kutosha kutokana na mapato ya milangoni, lakini hawakufanya vizuri. Kuhusiana na kelele za mashabiki kwamba waondoke, kiongozi huyo alisema wameunda kamati ya watu wanne ikiongozwa na Aziz Kifile na Ally Sule kuangalia mfumo wa klabu hiyo.
“Watu wanapiga kelele viongozi waondoke, timu iuzwe, hakuna mtu ambaye amekataa, sasa mpira una gharama kubwa, waliocheza zamani ilikuwa ni kujitolea sasa hivi hicho kitu hamna. “Wafadhili kidogo mechi kubwa mgawo Sh milioni nne, fedha za wadhamini Sh milioni 36, mahitaji Sh milioni 70 hapo ni kuendesha kimasikini, mishahara ya wachezaji. “Tumeunda kamati ya watu wanne itaongozwa na Aziz Kifile na Ally Sule kuangalia uwezekano wa kubadili mfumo kama ni wa hisa au la tumeipa mwezi mmoja, wanachama ndio mtaji pekee,” alisema Aveva.
Pia Aveva aliilamu TFF katika upangaji ratiba na kushusha lawama kwa waamuzi kwamba baadhi walikuwa mizigo na pia kulalamikiwa suala la wachezaji Amis Tambwe na Donald Ngoma wa Yanga kwamba walipeleka malalamiko TFF, lakini hayakufanyiwa kazi
Previous
Next Post »