NI kama mkosi, kwamba timu zote tatu zilizokuwa zinashiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, zimeshuka rasmi daraja. Ndizo zilizoshika nafasi tatu za mwisho katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16 na ambazo bingwa wake msimu huu ni Yanga iliyoweka rekodi ya kutwaa kwa mara ya 26 taji hilo tangu kuanzishwa kwa ligi nchini mwaka 1965.
Simba inafuatia kwa kutwaa mara 18. Matokeo ya kushuka rasmi kwa timu hizo yalifahamika jana baada ya matokeo ya mwisho ya mechi nane za kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2015/2016 zilizochezwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Wakati timu hizo zote za Tanga zikitoa mkono wa kwa heri, Azam FC imemaliza katika nafasi ya pili huku ikiacha Simba katika nafasi ya pili baada ya vijana hao wa Msimbazi jana kufungwa 2-1 na JKT Ruvu ya Pwani.
Mgambo JKT imemaliza ikiwa na pointi 28, huku African Sports 26 na Coastal 22. Ushindi wa Pili AZAM FC imeipiku Simba kwa kumaliza nafasi ya pili baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilizopigwa kwenye viwanja tofauti jana.
Kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Azam walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Mgambo JKT ya Tanga, sare ambayo haikuisaidia Mgambo kuepuka kushuka daraja. Sare hiyo iliisaidia Azam ambayo ilikuwa ikiombea Simba ifanye vibaya ili wenyewe waweze kumaliza katika nafasi ya pili.
Bao la Azam FC lilifungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ katika dakika ya 60 huku lile la kusawazisha la Mgambo JKT lilipachikwa na Fully Maganga katika dakika ya 72. Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 64, ikifuatiwa na Simba SC inayomaliza ikiwa na pointi zake 62 katika nafasi ya tatu.
Uwanja wa Taifa
Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wenyeji Simba walimaliza vibaya baada ya kupokea kichapo cha kufungwa mabao 2-1 na JKT Ruvu na kuifanya ishindwe kumaliza katika nafasi ya pili.
Mabao ya washindi yaliwekwa kimiani na Abdulrahman Mussa katika dakika ya kwanza na ya 30 ya mchezo huo, ambao ulipooza, huku lile la Simba likifungwa na mkongwe Mussa Hassan Mgosi katika dakika ya 70.
Majimaji Songea Yanga ambayo tayari ilishatwaa ubingwa na kukabidhiwa taji lake siku kadhaa zilizopita, jana ilimaliza kwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Majimaji katia mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea hivyo kufikisha pointi 73.
CCM Kirumba Mwanza
Mechi nyingine za kufunga pazia la Ligi Kuu, wenyeji Toto Africans walijikuta wakichapwa bao 1-0 na Stand United katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Bao hilo pekee la Stand United liliwekwa kimiani na Hassan Seif `Banda’ katika dakika 74 akisaidiwa na Amri Kiemba. Toto Africans walifanya shambulizi la nguvu moja tu ambalo hata hivyo liliokolewa na kipa wa Stand United.
Mkwakwani Tanga
Wenyeji Coastal Union ya Tanga ambao tayari walikuwa wameshashuka daraja, jana walisokomezwa zaidi shimoni baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tanzania Prisons ya Mbeya.
Sokoine Mbeya
Mbeya City ya Mbeya jana ililazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Ndanda FC katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Manungu Turiani
Mtibwa Sugar wameibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 baada ya kuichapa African Sports katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani. Kambarage Shinyanga Kagera Sugar walimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara vizuri baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya vijana wa Jamhuri Kiwelo `Julio’, Mwadui FC ya Shinyanga.
ConversionConversion EmoticonEmoticon