DC Kinondoni acharukia uchafu


MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amewaagiza maofisa biashara wa wilaya hiyo kumpa taarifa ndani ya saa sita kuanzia jana mchana, iwapo nyumba za kulala wageni mbili bubu na ghala moja lililokuwa limehifadhi bidhaa mbalimbali ikiwamo sukari, zinaendeshwa kihalali au la.
Alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Manzese TipTop, Dar es Salaam alikokagua nyumba ya kulala wageni ya Lambo Motel na kujionea uchafu uliokithiri, ikiwa ni pamoja na maji yaliyotuama na kutoa harufu, pia vyumba vichafu.
Hapi aliyefuatana na polisi, pia alijionea uchafu ndani ya vyumba hivyo inayodaiwa kushamiri kwa biashara ya ngono ambayo haikubaliki kisheria.
Sambamba na hilo, ameagiza kuanzia sasa polisi wawakamate madada poa wanaojiuza katika nyumba hiyo na maeneo mengine ya wilaya ya Kinondoni na kusema biashara hiyo imekuwa ikihusisha watoto wadogo jambo ambalo ni hatari na kusema halipaswi kuvumilika.
“Kuanzia sasa dada poa wote wanaojiuza hapa na maeneo mengine ya wilaya hii wote wakamatwe, biashara wanayofanya ni haramu, ziko biashara halali nyingi wakafanye, ila hii inayowahusisha pia hata watoto wadogo, hatuwezi kuvumilia,” alisisitiza Hapi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya alivamia ghala moja eneo jirani na hapo na kuamuru lifunguliwe jambo ambalo ndani yake kulikuwa na bidhaa nyingi zimehifadhiwa ikiwemo mifuko kadhaa ya sukari.
Previous
Next Post »