Serengeti Boys yaizima India



TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ jana iling’ara baada ya kuifunga India katika mashindano ya vijana yanayoendelea nchini India. Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka India, mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na Maziku Amani aliyefunga mawili kipindi cha kwanza na Asad Ali, ambapo hadi mapumziko Serengeti Boys ilikuwa mbele kwa mabao 2-1. Michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka India (AIFF) ili kuipa mazoezi timu yake, ikishirikisha timu mbalimbali duniani na inafanyika Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa, India. AIFF imeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka kesho. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika mwishoni mwa wiki, Serengeti Boys ilitoka sare ya 1-1 na Marekani, ambapo Jean Julien aliifungia Marekani dakika ya tano tu na Mohammed Abdallah akaisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 19.
Previous
Next Post »