Simba kuwakabili 'Wanalizombe' leo

 WEKUNDU wa Msimbazi Simba wanashuka uwanjani leo kucheza na Majimaji, mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakayopigwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Simba wataingia uwanjani leo huku wakiwa na kumbukumbu mbaya baada ya mechi iliyopita dhidi ya Mwadui FC kukubali kichapo cha bao 1-0.

Hata hivyo maandalizi ya mechi ya leo yalianza kwa gundu, baada ya wachezaji wake wote wa kimataifa kugoma kusafiri wakishinikiza kulipwa mishahara yao.

Baada ya uongozi wa Simba kuweka mambo sawa, wachezaji wawili kati ya saba waliogoma kusafiri na timu juzi kwenda Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya mchezo huo aliondoka jana.

Wachezaji hao ni kipa Vincent Angban raia wa Ivory Coast na kiungo Mzimbabwe Justice Majabvi ambao waliondoka kwa basi jana asubuhi.

Wawili hao waliondoka baada ya kikao cha pamoja baina ya wote waliogoma na Rais wa klabu, Evans Aveva kilichofanyika jana mjini Dar es Salaam.

Kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi amekwenda Songea leo asubuhi kuiongezea nguvu Simba.

Wachezaji hao waligoma kwa sababu ya kucheleweshewa mishahara ya Aprili na uongozi wa Simba ulisema juzi mishahara imechelewa kwa sababu wadhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hawajatoa fedha.

Wengine waliogoma ni beki Mrundi Emery Nimubona, kiungo mzawa Mwinyi Kazimoto, Waganda beki Juuko Murshid, kiungo Brian Majwegga na mshambuliaji Hamisi Kiiza.

Mbali na hao waliogoma Simba leo itawakosa pia viungo Jonas Mkude, Awadhi Juma na washambuliaji Ibrahim Hajib na Raphael Kiongera, ambao nao hawajasafiri na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa majeruhi na kutumikia adhabu za kadi.

Akizungumzia mechi ya leo, Kocha Mkuu wa Simba Jackson Mayanja alisema ni mechi ngumu lak ini watapambana.

"Tutapambana ingawa ni mechi ngumu, pamoja na kasoro zilizojitokeza ndani ya kikosi changu, tutahakikisha makosa hayo hayajitokezi tena," alisema Mayanja.

Previous
Next Post »