Hans Poppe amchimba mkwara Ajib


MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Ajib hata akifanikiwa majaribio nchini Afrika Kusini, lazima afuate taratibu kwani ana mkataba na Simba hadi mwaka 2017.
Akizungumza na gazeti hili, Hans Poppe alisema Ajib aliomba ruhusa kwenda kwenye majaribio, lakini walimkatalia na kwamba pengine ndiyo sababu alitafuta kadi nyekundu dakika za mwisho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Mwadui FC mwishoni mwa wiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Mwisho wa yote alifanikiwa, itabidi kuomba ridhaa Simba,” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa yupo Cape Town, Afrika Kusini kwa shughuli zake na kwamba mchezaji huyo yupo jijini Johannesburg.
Mshambuliaji huyo aliondoka nchini juzi, siku moja baada ya kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 90 katika mchezo ambao Simba ilifungwa bao 1-0 na Mwadui ya Shinyanga na kupoteza matumaini ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Kwa mara ya mwisho, Simba ilitwaa ubingwa msimu wa 2011/12. Wakati huohuo, uongozi wa Simba umemalizana na wachezaji wake wa kigeni waliokuwa wamegoma kusafiri na timu hiyo kwenda Songea mkoani Ruvuma kucheza na Majimaji ya huko kesho, kutokana na kutolipwa mshahara wao wa Aprili.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo zilieleza kuwa juzi kulikuwa na kikao kati ya wachezaji hao na Mwenyekiti wa Simba, Evans Aveva na kwamba jana wachezaji wawili, kiungo Justice Majabvi na kipa Vincent Angban waliondoka jana kwenda Songea kuongeza nguvu.
Wengine waliogoma ni Hamisi Kiiza, Brian Majwega na Juuko Murshid wa Uganda, Emiry Nimubona wa Rwanda na Mkenya, Raphael Kiongera.
“Imebidi tushinikize, sisi tuna familia zetu na tupo Simba kwa ajili ya kusaka fedha sio kuuza sura, wengine tunajua kabisa hatutakiwi tena, tunajua kuna mgawanyiko kwa viongozi, tunasubiri ligi iishe ili tumalizane kwa amani,’’ alisema mmoja wa wachezaji hao
Previous
Next Post »