TRA wapania kuvuka lengo la makusanyo


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema imedhamiria kutumia kipindi cha miezi miwili iliyobaki kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016 kukusanya Sh trilioni 1.4 ili kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka huu.
Lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ni Sh trilioni 12.3 ambapo katika kipindi cha miezi 10 kuanzia Julai, mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu imekusanya Sh trilioni 10.92 ambayo ni asilimia 99 ya lengo la makusanyo yote.
Hayo yameelezwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Alphayo Kidata wakati akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mwenendo wa makusanyo ya kodi kwa mwezi Aprili, mwaka huu.
Alisema bado wanaendelea na jitihada za kuhakikisha wanafikia na kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2015/2016 unaoisha Juni, mwaka huu.
“Katika kipindi cha mwezi Aprili, tumekusanya Sh trilioni 1.035 ambayo ni sawa na asilimia 99.5 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 1.040 katika mwezi huo wa Aprili,” alisema Kidata.
Alisema hatua hiyo inatokana na wafanyabiashara na wananchi kuwa na mwamko wa kutumia mashine za kielektroniki za kodi (EFDs) na kuwadhibiti wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine hizo kwa kuwakamata na kuwatoza faini.
Previous
Next Post »