Shamba la Kitulo kurejeshwa kwenye hali yake - Serikali


WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, amemweleza Mkuu wa Wilaya ya Makete, Daud Yassin kwamba serikali bado inafanya jitihada kuhakikisha shamba la mifugo la Kitulo linarejea katika hali yake.
Mwigulu alitoa kauli hiyo mjini hapa alipoonana na Yassin aliyekwenda kumkumbusha juu ya ahadi aliyoitoa wakati alipotembelea shamba hilo la mifugo Machi mwaka huu. Shamba hilo lililoanzishwa mwaka 1995 la ukubwa wa hekta 5,000, lina uwezo wa kufuga ng’ombe zaidi ya 4500 lakini sasa lina wachache na vitendea kazi vimeharibika.
Kwa mujibu wa Yassin, Waziri Mwigulu amesisitiza kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha linarejea katika hali yake na kuchangia kukuza pato la taifa. “Nimezungumza na Waziri na amenieleza nia ya serikali kulirejesha shamba la Kitulo katika hali yake,” alisema Yassin.
Waziri alisema tayari wizara yake imeanza kuangalia njia mbalimbali zitakazowezesha kutatua matatizo yaliyopo kwa sasa katika shamba hilo. Nia ya serikali ni kuimarisha shamba la Kitulo ili kuwapa mafunzo ya ufugaji wa kisasa wafugaji wa Nyanda za Juu Kusini wafuge badala ya kuchunga. Yassin alisema, endapo serikali itatatua matatizo yaliyopo shambani hapo, tija itaongezeka kwa kuwasaidia wananchi na kuchangia pato la taifa
Previous
Next Post »