Yanga yajibeba 2015/16


YANGA imefikisha pointi 71 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa na mechi mbili mkononi na imejihalalishia sherehe zake za ubingwa.
Hatua hiyo inatokana na ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata jana katika mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imejihalalishia ubingwa baada ya mapema jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas kutoa taarifa kuwa timu ya Azam FC imekata rufani kupinga kupokwa pointi tatu na mabao mawili dhidi ya Mbeya City mchezo wa Februari mwaka huu.
Ingawa Yanga kimahesabu ilishatwaa ubingwa tangu Jumapili baada ya Simba iliyokuwa na uwezo wa kufikisha pointi 70 kama ingeshinda michezo yake iliyobakia kufungwa bao 1-0 na Mwadui, lakini uamuzi wa Azam kukata rufani ulionekana kubadili upepo kama itashinda rufani hiyo.
Azam inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16 ikiwa na pointi 60 na kama itashinda mechi zake mbili zilizobaki itafikisha pointi 66.
Lakini kama Azam itashinda rufani yake na kurudishiwa pointi tatu ilizopokwa kwa kumchezesha Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano, itafikisha pointi 69, hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuchelewesha ubingwa wa Yanga, lakini kwa matokeo ya jana vijana hao wa Jangwani hakuna kitakachowazuia wasisherehekee mapema ubingwa wao msimu huu. Pia matokeo ya jana yameifanya Mbeya City ibaki nafasi ya nane ikiwa na pointi 33, nayo ina michezo miwili mkononi kumaliza ligi hiyo msimu huu.
Katika mchezo wa jana Yanga ilipata bao dakika ya 15 mfungaji akiwa Vincent Bossou kwa kichwa akitumia vyema krosi ya beki Juma Abdul, wakati bao la pili lilifungwa na Amis Tambwe dakika ya 85.
Kwa bao hilo, Tambwe amefikisha mabao 21 akiendelea kuongoza katika orodha ya wafungaji bora msimu huu na kumuacha Hamis Kiiza wa Simba akimfuatia akiwa na mabao 19.
Katika mchezo huo Yanga ililazimika kufanya mabadiliko mara mbili kipindi cha kwanza, ambapo mara ya kwanza ilikuwa dakika ya nane wakati Mbuyu wite alipoumia na nafasi yake kuingia Salum Telela.Dakika ya 30 Yanga ilifanya tena mabadiliko kwa kumtoa Bossou aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Kelvin Yondani.
Wachezaji wa Mbeya City wakiongozwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Salvatory Nkulula na Joseph Mahundi mara kadhaa walijitahidi kulifikia lango la Yanga lakini umaliziaji haukuwa mzuri.
Nao washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Donald Ngoma na Amis Tambwe kwa nyakati tofauti walifanikiwa kuingia katika eneo la hatari la Mbeya City, lakini walishindwa kulenga lango ama mipira yao kuokolewa na kipa Juma Kaseja
Previous
Next Post »