Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , William Lukuvi aliwasilisha bajeti yake juzi Jumamosi na kujadiliwa na wabunge hadi saa nane mchana, na mjadala huo utaendelea kabla ya kuhitimishwa leo jioni.
Katika hotuba yake, Lukuvi alizungumzia hatua nyingi zitakazofanyika kutatua kero za ardhi ikiwamo kuanzisha ukomo wa miliki ya ardhi na kuandaa programu ambayo ndani ya miaka mitano inatarajiwa kumaliza migogoro ya ardhi nchini.
Baada ya mjadala wa Ardhi kukamilishwa leo jioni, kesho itakuwa zamu ya Profesa Jumanne Maghembe wa Maliasili na Utalii. Tayari baadhi ya mambo kuhusu maliasili na utalii, yamezungumzwa katika mjadala wa ardhi ambako wabunge wamelalamikia hatua ya wizara kuondoa mifugo katika baadhi ya maeneo ya hifadhi.
Kumekuwa na changamoto kubwa ya matumizi ya ardhi, ambayo imesababisha wafugaji na wakulima kuvamia maeneo ya hifadhi kinyume cha sheria. Profesa Maghembe anatarajiwa kuzungumzia hilo kwa kina kutokana na kuwapo dalili za wabunge kumbana kueleza hatua zinazochukuliwa na wizara yake katika mjadala utakaodumu kwa siku mbili.
Profesa Joyce Ndalichako atakuwa kilingeni kwa siku mbili kuanzia Alhamisi atakapowasilisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Katibu Mtendaji huyo wa zamani wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), atakuwa ni mara yake ya kwanza kuwasilisha bajeti bungeni, na wengi wanasubiri kuona alichokuja nacho akiongoza sekta ya elimu katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Serikali ya Awamu ya Tano imeanza vizuri kwa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne kuanzia Januari mwaka huu. Zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu, ingawa mafanikio makubwa ikiwamo uamuzi huo wa kuondoa michango iliyokuwa kero kwa wananchi, hivyo kuipatia sifa serikali.
Wizara ya Maji na Umwagiliaji itakamilisha wiki Jumamosi kwa Waziri Gerson Lwenge kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi bungeni. Sekta ya maji ni moja ya sekta inayogusa maisha ya kila siku ya watu ikitarajiwa mjadala wake wa hadi Jumatatu ijayo, kuvutia wabunge wengi kuchangia. Wiki iliyomalizika, Bunge lilipitisha bajeti za wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Nishati na Madini.
ConversionConversion EmoticonEmoticon