Samia: Sijawahi kupinga utumbuaji majipu


MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu amewataka wakuu wa mikoa na wa wilaya, kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma wanapotaka kufukuza kazi watumishi wanaokwenda kinyume. Samia alisisitiza jana kuwa hajawahi kupinga utumbuaji majipu kama ambavyo alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Hata hivyo, aliwaambia wakuu hao wa mikoa na wilaya kwamba mwenye mamlaka ya kutumbua majipu ni Rais pekee, kwa kuwa anateua, anaajiri na kufukuza. Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha juu ya agizo lake la kutaka mifugo iliyo ndani ya hifadhi za Taifa (Tanapa) ihamishwe.
Alisema wakuu wa mikoa na wilaya nchini, wanapaswa kuhakikisha wanapotaka kuwajibisha watumishi wa umma wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Rais pekee ndiye ana mamlaka ya kuteua, kutengua na kuajiri; Lakini sijapinga utumbuaji wa majipu bali nasisitiza kila RC (Mkuu wa Mkoa) na DC (Mkuu wa Wilaya) afuate sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma,” alisema. Makamu wa Rais alisisitiza mifugo inayotoka nje ya nchi iliyomo kwenye hifadhi za taifa, kuhakikisha inaondolewa ifikapo Juni 30.
Previous
Next Post »